Sunday, October 28, 2012

MKARIBISHE YESU KWENYE CHOMBO CHAKO.

Na Mch.: Mwangasa (RP-Resident Pastor)

Mathayo 14:22-33, Yesu alikuwa akiendelea kutenda kazi alizokuja kuzifanya duniani na ukisoma kuanzia Mathayo 14:1-… Utaona aliwalisha watu elfu tano (waume). Na wakati watu wakitaamaki akawalazimisha wanafunzi wake kupanda chomboni ili wavuke bahari. Wanafunzi wake walipokuwa katikati ya bahari ndipo ilipotokea upepo mkali na kuanza kusukasuka chombo. Tuna mambo mengi ya kujifunza kupitia maandiko haya:-

HALI YA WANAFUNZI KATIKA CHOMBO:
Ukitafakari kwa makini utaweza kuona hali ya wanafunzi chomboni; inawezekana walishaanza kumlaumu Yesu, au kumlaumu kwa kuwalazimisha kupanda chomboni na yeye asiwemo.

Pia, wanafunzi wa Yesu walikuwa wamekata tama, kwasababu tukio hili lilipotokea mwanzo walikuwa na Yesu chomboni akaukemea upepo lakini mara hii Yesu hakuwepo chomboni. kwa maana hiyo wanafunzi walikuwa katika hofu kuu.

Biblia inasema hata wanafunzi walipomuona Yesu akitembea juu ya maji, wakahisi ni kivuli chake. hapa tunajifunza kuwa kuna wakati kwenye maisha unaweza kuwa unapita kwenye hatua ngumu kimaisha, na kwasababu ya hofu ukajikuta unaiogopa njia ambayo ndio ufumbuzi wa tatizo lako.

KWANINI YESU ALITEMBEA JUU YA MAJI:
Yawezekana umejiuliza kwanini Yesu alikuja huku akiwa juu ya maji; Kimsingi bahari ndio ambayo ilikuwa tatizo kwa wanafunzi wake, kwahivyo Yesu alikanyaga bahari kuonyesha kuwa lile tatizo lilikuwa chini ya miguu ya Yesu. Kumbe Yesu yupo juu ya tatizo linalokuzunguka maana lipo chini ya miguu yake.

Na ndio maana Petro naye alijaribu kupita juu ya tatizo yaani bahari lakini alipoiangalia bahari alipata hofu. HAPA tunajifunza jambo kwamba hatakiwi kuliangalia tatizo bali mwangalie Yesu ambaye yupo juu ya tatizo.

Ukimwamini Yesu unavuka kutoka mautini unaingia uzimani, na Yesu ana mamlaka na funguo za mauti na kuzimu. Hivyo ukiwa kwenye tatizo, usiangalie tatizo bali mwangalie Yesu. unapoelekea kwa Yesu usipepese macho, mtazame Yesu aliyekufa msalabani kwaajili yako.

JAMBO LA KUFANYA UKIWA NDANI YA TATIZO:
Katikati ya bahari wanafunzi wakamuona Yesu kama tumaini lao, na ndipo Petro alipoamua kumfuata. kimsingi uamuzi wa Petro kumfuata Yesu kwa kutembea juu ya maji ni sahihi kabisa, ila tatizo ni kwamba petro alitumia uzoefu wake wa bahari ambao ukamfanya asiwaze sauti ya Yesu aliyemuita. watu wengi wameshindwa kutoka ndani ya tatizo kwasababu ya taarifa walizozisikia kutoka kwa watu.

Mfano; Mtu ana tatizo la ndoa na ndio limeanza, lakini baada ya kuongea na mtu mwengine mwenye tatizo kama hilo, anamwambia kuwa amedumu kwenye tatizo hilo kwa miaka mingi. Taarifa hiyo moja tu inamfanya huyu ambaye tatizo la ndoa ndio limeanza, akate tamaa na kuingiwa na hofu kabisa kwa kuhisi naye atadumu kwa miaka hiyo yote.

Ni muhimu kujua hakuna haja ya kuangalia tatizo wala watu wengine waliopo kwenye tatizo. tunatakiwa tumuangalie Yesu Kristo ambaye aweza kukutoa kwenye tatizo ulilonalo. unapomwita Yesu kwenye mwili wako uliojaa magonjwa atakapofika yeye yote yatakoma, ukimwita Yesu kwenye ndoa yako yenye matatizo atakapofika tatizo litakama.

Isaya 41:9-10 “wewe nilikushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwamaana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.” Kama ukijua jambo ambalo Mungu anataka utend kwenye tatizo utalibadili tatizo hilo na kuwa daraja la kukuvusha na kukupeleka kwenye hatma njema ya maisha yako.

Maombi:
Baba Mungu katika Jina la Yesu Kristo leo nimetambua kuwa ninatakiwa nitakiwa nikutazame wewe ninapokuwa kwenye tatizo. ninaomba msamaha kwasababu ya kutazama mambo mengine badala kukutazama wewe Mungu, Mungu naomba unisamehe katika Jina la Yesu.

Katika Jina la Yesu nimeamua kukuita wewe leo, imeandikwa katika Yeremia 3:33 “niite, nami nitakuitikia, name nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Leo ninakuita katika Jina la Yesu. Mungu kutoka katika kiti chako cha enzi ninakuita katika Jina la Yesu. Ninakutumaini wewe Mungu katika Jina la Yesu. Natakanivuke na wewe Mungu hadi ng’ambo ya maisha yangu katika Jina la Yesu.

MWITE YESU KWENYE TATIZO ULILONALO!!!

No comments:

Post a Comment