Wednesday, January 23, 2013
UPINZANI UNAPOTOKEA KUPINGA UAMSHO NA WOKOVU, BIBLIA INAKUSHAURI UFANYE NINI?
Mara nyingi upinzani unaotokea unakuwa katika maeneo ya kupinga uamsho, kupinga wokovu, kupinga mafundisho ya kweli, kupinga miujiza ya kweli ya Mungu inayotokea na pia, kuwapinga watumishi wa Mungu wanaotumiwa na Mungu katika uamsho.
Katika jibu la swali la mwezi huu ningependa nikuwekee mistari mbalimbali kutoka katika Biblia inayotushauri tuwe tunafanya nini unapotokea upinzani dhidi ya uamsho.
Ni vizuri kujua ya kuwa si kila mtu anakubaliana na mambo ya uamsho, pia si kila dhehebu la kikrsto linakubaliana na uamsho wa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo ni vizuri ujiandae na ujue cha kufanya unapokutana na upinzani.
Unaposongwa na upinzani Biblia inakushauri ufanye yafuatayo:
1. FURAHI WALA USIKASIRIKE! (Mathayo 5:11,12; I Petro 4:12-16):
"Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi, na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili (ya Yesu) yangu. Furahini na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu’’.
‘’Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoshiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe. Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia. Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine. Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo (au ikiwa kwa sababu ameokoka) asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo”.
2. BARIKI WALA USILAANI! (Warumi 12:14; Luka 6:28, I kor 4:12,13)
"Wabariki wanaowaudhi, barikini, wala msilaani pia, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi’’.
Mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho jinsi wao walivyofanya anasema; “tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi’’.
Na wewe fanya kama Mtume Paulo ukitukanwa kwa sababu ya kuokoka bariki, ukiudhiwa kwa sababu ya wokovu stahimili au vumilia, ukisingiziwa uongo, jifunze kujibu kwa hekima!
3. TENDA WEMA USILIPIZE KISASI! (Warumi 12:17,18; Waebrania 12:14,15; Warumi 12:19-21; Luka 6:27
"Msilipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo’’.
‘’Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu(mwachie Mungu jambo hilo linalokuletea hasira); maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu mimi, mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema’’.
‘’lakini nawaambia ninyi mnaosikia wependeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi.’’
4. WAOMBEE WANAOWAUDHI! Luka 6:28b; Mathayo 5:43-45, Mathayo 26:41)
‘’Waombeeni wale ambao wawaonea ninyi’’. ‘’Mmesikia kwamba menenwa, umpende jirani yako, na umchukie adui yako, lakini mimi (Yesu) awaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki’’.
“ Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribu; roho ii radhi, lakini mwili ni dhaifu’’.
5. USIKATISHWE TAMAA ENDELEA KUFANYA ANALOKUAMBIA MUNGU KATIKA UTII NA HEKIMA! (Warumi 16:17-19)
‘’Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza (ya kweli); mkajiepushe nao. Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu. Maana utii wenu umewafikilia watu wote… lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya. Naye Mungu wa amani atamseta shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi’’.
6. WASHIRIKISHE WATEULE WENZAKO WAKUOMBEE KATIKA UPINZANI UNAOKUZUNGUKA! (Warumi 15:30-32).
Ndivyo Mtume Paulo alivyofanya alipowaandikia wateule wenzake aliposema;
‘’Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi’’.
Yamkini Mungu atajibu maombi ya wateule hao wakiomba kwa imani na kwa bidii juu yako. Kitabu cha Matendo ya Mitume sura ya 12 kinatueleza jinsi ambavyo Mtume Petro alipokumbwa na upinzani hata akafungwa-lakini (Kanisa) wenzake waliokoka waliomba kwa juhudi kwa ajili yake na Mungu akamfungua toka gerezani.
7. JIEPUSHE NA MABISHANO! (Tito 3:9; Wakolosai 4:5)
Mara nyingi upinzani wa wokovu na mambo ya uamsho unapotokea-kunatokea pia maswali na mabishano yasiyokuwa na msingi wala maana yoyote. Wengi bila kujua wamejikuta wameingia katika majibizano na mabishano juu ya wokovu na neno la Mungu. Biblia inasema hivi:
‘’Lakini maswali ya upuuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria (Neno la Mungu). Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana’’ enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu’’.
8. USIKATE TAMAA, VUMILIA MPAKA MWISHO! (I Petro 3:13-17; Mathayo 24:13)
‘’Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu’’.
Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya’’. ‘’lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka’’.
9. USIONE HAYA- SONGA MBELE KATIKA WOKOVU (Waebrania 12:1-3; I Petro 4:15,16)
‘’Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu’’. ‘’Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine. Lakini ikiwa kwa sababu ni mkristo (au ameokoka) asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo’’.
10. USIJIULIZE – ULIZE UTAKACHOJIBU! (Marko 13:9,11)
‘’Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa;; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili (ya Yesu), kuwa ushuhuda kwao …. Na watakapowachukuwa ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakavyosema, lakini lolote mtakalopewa saa ile, lesemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu’’.
11. MUWE NA KIASI NA KUKESHA! (I Petro 5:8-9; Yakobo 1:2-4; Yakobo 4:7; I Petro 5:10)
‘’Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka – zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani…’’ ‘’Ndugu zangu, hesabuni yakuwa ni furaha tupu, mkiangikia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi (uvumilivu). Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno’’. ‘’Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani, naye atawakimbia’’.
“ Na Mungu wa neema yote aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu’’.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment