Na Mch. Maximillian Machumu
Mchungaji Maximillian Machumu (RP) akihubiri jumapili hii
Waamuzi 15:9-16: Samson alikuwa mnadhiri wa Mungu na aliwekwa kuwaangamiza wafilisti, kwasababu ya kuwaangamiza Wafilisti ndugu zake wakaamua kumfunga na kumkabidhi kwa wafilisti ili wasije kulipa kisasi kwa wao. Katika kumfunga Samsoni, ndugu zake wapatao elfu tatu walitumia kamba mbili; kuna mambo mengi ya kujifunza kupitia habari hii ya Samsoni:
KWANINI NDUGU WALIMFUNGA: kama tulivyosoma katika kitabu cha Waamuzi 15:9-16, ndugu zake ndio waliohusika kumfunga Samsoni. Hapa tunajifunza kuwa mara nyingi adui (shetani) anapotaka kumfunga mtu hupitia kwa watu wake au wanaomjua mtu huyo vizuri. Kifungo kinachotokana na watu wako wa karibu ni kibaya zaidi kwasababu wanaujua udhaifu wako; muda gani unaomba na muda gani huombi.
Ndio maana hata Mtume Paulo aliwahi kutegeshewa nyoka kwenye kuni (Matendo ya Mitume 28:3). Nyoka ni yule mtu wa karibu anayejua siri na mambo unayoyafanya, kwasababu hiyo inakuwa rahisi kwa shetani kuwatumia kukuangamiza. Nyoka hakuonekana mwanzoni kwa Paulo kwasababu alijifanya kama kuni, na watu wa karibu ni vivyohivyo huwezi kuwatambua kwa urahisi. Furaha ni kuwa Mungu hakuruhusu yule nyoka kumwangamiza Mtume Paulo.
KWANINI WALITUMIA KAMBA MBILI: Ndugu wa Samsoni walikuwa elfu tatu lakini jambo la ajabu ni kuwa walibeba kamba mbili tu; Utajiuliza nini siri ya hizi kamba mbili?. Yesu mwenyewe aliainisha kamba mbili kuu ambazo shetani anazitumia kuwaangamiza na kuwafunga watu duniani. Ukisoma katika Ufunuo 1:18 “na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.” Kumbe zile kamba mbili zina maana ya mauti na kuzimu. Kuzimu inaleta magonjwa na matatizo mbalimbali lakini mauti inaleta kifo. Kamba mbili mpya ni mauti na kuzimu. Kwa kuzimu na mauti shetani amekuwa akiwaangamiza na kuwatesa watu wa Mungu. Inawezekana na wewe ni mmoja wa watu wanaoteseka kwasababu ya kamba hizi leo kuna habari njema kuwa Yesu aweza kukata kamba hizo.
MATOKEO YA KIFUNGO CHA SAMSONI: baada ya kumfunga, ndugu zake wakamkabidhisha kwa wafilisti yaani adui zake. Jambo la ajabu likatokea, mara baada ya kukabidhiwa. Imeandikwa, “Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake.” Waamuzi 15:14 kupitia kifungo kile Mungu akamtumia Samsoni kuwaangamiza wafilisti wote. Kumbe waweza upo katika kifungo ambacho Mungu alikiruhusu ili upate ushindi ulio mkamilifu.
MUNGU ANAWEZA KUKATA KAMBA ZILIZO KATIKA MAISHA YAKO: Wachawi na waganga wanaweza kuwa wajanja mbele ya macho yetu lakini Bwana anawaona, na kamba zao zinaonekana mbele ya macho ya BWANA. Hata mfalme Daudi aliwahi kuwa katika kamba hizo ukisoma katika Zaburi 119:61 “Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako.” Upo uwezekano wa mtu kufungwa, Mwilini unajiona ni mtu asiye na mafanikio au asiye na mwelekeo lakini rohoni unakuwa umefungwa na kamba kabisa. Zaburi 18:1->… “…Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake…” Mungu anaweza kukutoa katika kamba za matatizo unayopitia. Daudi alipokuwa katika kamba hizo aliliitia jina la BWANA.
Yesu alipofufuka akatangaza kuwa anazo funguo za mauti na kuzimu, Hata kama aliyekufunga awe mtu wa karibu kiasi gani lakini zipo funguo za kufungua kamba zilizokufunga. Kama alivyofanya kwa Samsoni; baada ya kukufungua kinachofuata ni kipigo kwa wale wote walioshiriki kukufunga. Mungu anaweza kukutofautisha; shida na mateso yote unayopitia si kitu mbele za Mungu wetu kwasababu yeye anaweza kukuweka huru. Mpokee Yesu upate uhuru mkamilifu, kwasababu dunia ya leo haipo salama kama haupo ndani ya Yesu.
Sunday, March 10, 2013
Saturday, March 9, 2013
FAHAMU NINI MAANA YA KUSIFU NA KUABUDU KATIKA BIBLIA
Nini maana ya kusifu na kuabudu
KUSIFU NA KUABUDU ni maneno
tofauti na yana maana tofauti
1. kusifu
MAANA --- nikuelezea wasifu au
wajihi za kitu au mtu. Sasa
tunaposema tunamsifu Mungu
inamaanisha ni KWA KUMUINUA
JUU, KUSHUKURU KUMPAZIA
SAUTI,KUFANYIA SWANGWE,
KUJISHUSHA CHINI YAKE KWA
UNYEYEKEVU,nk Zaburi 100:4
Neno hili kusifu kwa kiebrania
lilikuwa na maana ya;
Tehila, yaani kutamka neno kwa
kuongeza vionjo na mbwembwe
zaidi. Mfano neno haleluya
unalitamka (Ha, ha leluya huuu eee)
Tehila ni kuwa kama kichaa
unaposifu au kuabudu kwa utukufu
wa Bwana. (Nilidhani labda hapa
ndipo waswahili walipopata neno
taahila).
Yadaa yaani kujiachia kwa Mungu
(you just surrender yourself to the
Lord).
Barak yaani kusaluti mbele za
Bwana. Ni kuonyesha kwamba ni
yeye peke yake anayestahili heshima
na utukufu. Huwezi kumpigia saluti
mtu usiyemwona, hivyo ni kwa njia
ya kumwabudu Mungu katika roho
na kweli ndipo tunapomwona kama
alivyo na utukufu wake
2. Kuabudu
Neno la Kiebrania shachah lina
maana ya kuabudu, kusujudia,
kuinama kwa kuonesha
unyenyekevu, kuonesha heshima
kubwa au kuanguka kifudifudi. Neno
la Agano la Kale proskuneo
halikadhalika lina maana ya kubusu
mkono, au kupiga magoti na kugusa
ardhi kwa paji la uso kwa
unyenyekevu mkuu. Maneno
mengine mawili ya kuabudu yana
maana ya kutumika, kufanya ibada
Takatifu na kumtolea Mungu Sadaka.
Waache Watu Wangu Waondoke, Ili
Wapate Kunitumikia, Dai hili Mungu
alilolirudia mara kwa mara lilipelekea
Farao kuwaruhusu watu wa Mungu
kutoka Misri. Tangu wakati huo,
Mungu, Mungu mwenye wivu,
amekuwa akipambana na watu wake
akiwazuilia kuabudu miungu mingine
na sanamu, na badala yake
wamwabudu Mungu aliye hai na wa
kweli. Kutoka 7:16
Ibada ni kumtukuza Mungu na
kumfurahia daima. Mungu
anawatafuta watu wa kumwabudu,
na kufanya ibada ndiyo wito wetu
wa kwanza (Yn4:23 Lakini saa yaja,
tena ipo, ambapo wale waabuduo
halisi, watamwabudu Baba katika
roho na kweli. Watu wanaoabudu
namna hii, ndio Baba anawatafuta.
Msitari wa 24 unasema Mungu ni
Roho na wote wanaomwabudu
imewapasa kumwabudu katika roho
na kweli.). Ibada ya kweli ni pale
tunapomruhusu Roho Mtakatifu
atuongoze kutoka katika roho zetu
au mioyo yetu kuabudu katika roho
na katika kweli na sio tumaini letu
ktk miiliau akili zetu Flp 3:3.
Ibada ni tendo la thamani kubwa, ni
la kipekee na linamhusu Mungu
(utatu mtakatifu) ambao peke yao
wanastahili. Lucifer, aliyekuwa
mhusika mkuu wa ibada huko
mbinguni, alitaka ibada hiyo iwe kwa
ajili yake, maana yake aabudiwe
yeye badala ya Mungu; na hilo ndilo
lililopelekea kuanguka kwake (Isaya
14 na Ezekieli 28). Hata wakati fulani
alitaka Yesu amsujudie ili eti ampe
falme zote za dunia lakini Bwana
alikataa Mt4:8-10.
Kwa hiyo kuabudu ni ibada na
tunaposema ibada sio zile taratibu
za kibinadamu tulizojipangia katika
ibada zetu za siku za leo, ibada za
leo tumeweka mambo mengi sana
na yanatumia muda mwingi sana
kuliko ile maana hasa ambayo
mungu aliikusudia katika agano la
kale utana ibada zilikuwa zinafaywa
kwa mambo makuu 2 neno la
Mungu, na Kuabudu.
Kuabudu ni sehemu ya maisha
wanadamu tumeumbiwa kuabudu,
watuwezi kuishi bila kuabudu hapa
haijalishi unaabudu nini!!! Unaweza
kuwa unaabudu Mungu wa kweli au
miungu kama ambavyo ukisoma bilia
utaona kuna miungu mingi inatajwa
mfano Baali, Dagon ink na hata leo
iko miungu mingi ambayo wanadamu
wanaiabudu lakini wa kuabudiwa ni
mmoja tu. Na katika biblia tunaona
kuaudu kwa mara ya kwanza
kulikofanywa na Ibrahimu kutoka
katika kitabu cha mwanzo 12: 8
Psalms 34:1 inaonyesha tunatakiwa
kumwabudu Mungu kila wakati.
Kwanini tuabudu
kuabudu ni agizo kutoka kwa Mungu
kutoka 20 2-4 . Psalm 96:9, Psalm
29:2 Tunapomwabudu mungu naye
Mungu hufurahiwa na sisi Zephaniah
3:17 Rom 12:1-2
Your Worship = Your View of God
jinsi unavyoabudu ndiyo mwonekano
wa mungu ulivyo ndani yako,
haijarishi unaabudu wapi uwe peke
yako au mko wengi kama unaabudu
kwa kutokumaanisha au kumaanisha
itajulikana tu na hivyo ndivyo mtu
anaweza kujua ni jinsi gani mtazamo
wako kwa Mungu wako.
KUNA NGUVU KATIKA KUSIFU NA
KUABUDU
Yoshua 6:20 Matendo 16:23-26
zinaonyesha ambavyo kwa kutumia
kusifu tu Mungu alishuka na kufanya
lile lililokuwa hitaji lao.
Kusifu kunamfukuza adui
Psalms 50:23. 2 Nyak 20:22. Ukiwa
unasifu na kuabudu humfukuza adui
mbali kutokana na ukiwa kwenye
ibada Mungu hushuka maana yeye
anasema anakaa katikati ya sifa
hivyo palipo na Mungu shetani
hawezi kuwepo lazima akae
mbali.akimbie mbali kabisa maana
kunakuwepo na uwepo wa bwana
wa Majeshi.
Je, ni wakati gani tuabudu?
Ni niyakati zote zinafaa kumwabudu
Mungu. Kwa nyakati zilizotengwa
Zaburi ya 100 inatuelekeza namna
ya kuanza, lakini zaidi ya yote
tunapaswa kuishi maisha ya ibada
bila kukoma. Kwa kila tunapopumua,
kwa kila wazo, kwa neno na tendo,
tunapaswa kumwabudu Mungu wetu
mzuri tunayemtumikia milele na
milele Zab 145:1,2
mwa 12:6- Siku zilipita na watu
wakafanyia ibada kwenye Hekalu na
kwenye masinagogi; lakini siku hizi
miili yetu ni hekalu la Mungu 1Kor
6:19 tu hekalu la Mungu sisi ibada
zinatakiwa zifanyike kila wakati na si
mara moja kwa wiki kama wengine
wanavyo dhani.
Je, Tunafanyaje Ibada?
Biblia inatufahamisha jinsi watu
walivyotumia mioyo yao, mawazo
yao, mikono yao, viganja vyao, miguu
yao, na midomo yao katika uimbaji.
Walipaza sauti zao kwa furaha na
kusujudu, kucheza, kusifu, kubariki
na kushukuru.
Maneno kama halal na haleluya
kutoka katika Zaburi yana maana ya
kusifu, kumwinua na
kumwadhimisha Bwana. Neno Yadah
lina maana ya kunyoosha mikono
hewani, na neno barak lina maana ya
kupiga magoti katika ibada ya
kumbariki Mungu. Kuitoa miili yetu
katika kumhudumia Mungu na
mwanadamu ni ibada pia (Rum
12:1). Watu pia humwabudu Mungu
katika sanaa zao, katika uandishi
wao, katika michezo ya kuigiza,
katika muziki, katika usanifu wa
majengo, na hata katika utoaji wa
fedha zao kwa ajili ya Injili.
Kusifu na kuabudu sio kuimba tu
Watu wengi wanajua kuwa kusifu na
kuabudu ni kuimba tu hapana kuna
njia nyingi za kusifu au kuabudu,
unaweza kutumia sanaa nyingine
kumwabudu mungu au watu
wengine wakamwabudu Mungu mf
maigizo, ngonjera, shaili, uchoraji,
upambaji au unakshi wa vitu,
kujenga .nk
Ibada Kanisani
KatIka kanisa makusanyiko yetu
yanapaswa kujawa na zaburi,
nyimbo, na tenzi za rohoni ambazo
zinaweza kuongozwa na Roho katika
lugha mpya anazotupatia Yeye.
Kwahiyo mikutano mingi ya kisasa
haina tofauti sana na burudani za
kikristo kama kwenye kumbi za
starehe. Watu huwa wanaangalia tu,
lakini je, wanaabudu? Uwepo wa
Mungu na Roho wake katika ibada
zetu utawafanya watu wasioamini
kuanguka chini na kuabudu (Kol
3:16) (1Kor 14:15,16,25,26) (Efe
5:19) (Mdo 2:4).
Ibada Ya Kweli Ina Gharama
Biblia inazungumzia habari za sadaka
za kusifu. Daudi alicheza mbele za
Bwana kwa nguvu zake zote, na
akakataa kumtolea Mungu kafara
ambayo isingemgharimu cho chote
(2Sam 6:14; 24:24). Wale mamajusi
wa Mashariki walitoa zawadi za
gharama kubwa walipokuja
kumwabudu Yesu (Mt 2:9-12), na
mwanamke mmoja alimpaka Yesu
kwa mafuta ya gharama kubwa,
akamwosha miguu yake kwa
machozi yake, na kuifuta kwa nywele
zake (Lk 7:36-50). Hivyo ibada
yoyote inaambatana na kutoa tena
vitu vyetu vya thamani.
Tunapaswa kumsifu Mungu kwa jinsi
alivyo na kwa matendo yake; lakini
Mungu mwenyewe anawatafuta na
anawataka wafanya ibada, na si
mradi ibada tu. Kusifu kwaweza
kufanywa hadharani, lakini ibada
mara zote ni jambo la ndani ya
moyo. Kusifu mara zote kunaweza
kuonekana au kusikika, lakini
kuabudu yaweza kuwa ya
kimyakimya na iliyofichika. Kusifu
kunaonekana, kuna kutumia nguvu,
kuna misisimko na furaha; lakini
ibada mara zote ni heshima na hofu
katika uwepo wa Mungu.
Biblia pekee inatuonesha jinsi
Mungu anavyo hitaji na kutamani
kuabudiwa na yeye pekee yake
ndiyo anayestahili kuabudiwa.
Kusifu na kuabudu kwa siku za
leo
Katika siku za leo kuna ufinyu wa
mafundisho katika kusifu na kuabudu
na ndiyo maana ya kuanda somo hili
ili tupanuane mawazo. Watu wengi
wa leo wanadhani kusifu ni kuimba
kwa nyimbo zenye midundo ya
harakaharaka(zouk&sebene) na
ukipunguza spidi ndo kuabudu.
Hasha tunaposema kusifu inatokana
na maneno yaliyopon kwenye
wimbo husika kweli ni ya kusifu,
kama ni maneno ya kusifu tunasema
ni wimbo wa sifa haijarishi speed
inayotumika na hali kadhalika
nyimbo za kuabudu. Watu katika
kipengele hiki huwa wanachakanya
nyimbo utakuta wakati wa kusifu
anaimba wimbo wa kutia moyo au
wa maombi, kinachotakiwa ni kujua
kuwa kila jambo lina wakati wake
ziiko nyimbo za mazishi, kufariji,
kutia moyo, za maombi, za kusifu ,
na za kuabudu nk sasa usichanganye
kwenye kusifu wewe unaimba
parapanda italia au tuonane
paradiso, hizo sio za sifa sasa najua
wewe utafanya zoezi la nyimbo
unazozijua ili kufahamu zina ujumbe
gani na ziko katika kundi lipi kati ya
hayo niliyokufundisha hapo juu.
Baadhi ya maandiko yanayo
onyesha aina za kusifu na
kuabudu kwa:
1. Kusimama (Zab 135:1-2, 134:1)
2. Kuinua mikono (Zab 134:2, 28:2)
3. Kuinama au kupiga magoti (Zab
95:6)
4. Kupiga makofi (Zab 7:1)
5. Kucheza (Zab 149:3, 150:4, 2Sam
6:14)
6. Kicheko (Zab 126:2, Ayu 8:20-21)
7. Kufurahi (Kumb 12:11-12, Law
23:40)
8. Kutembea (2Nya 20:21-22)
9. Shangwe (Zab 95:1)
10. Kupiga kelele (Zab 66:1, Law
9:23-24)
11. Kupiga vigelegele (Zab 33:1,
32:11)
12. Ukimya (Mhu 3:7)
13. Kupaza sauti (Isaya 12: 6, Zab
42:4)
14. Kulia/ kutoa machozi katika roho
mtakatifu
Mathayo 6:33 Utafuteni kwanza
ufalme wake na haki yake na hayo
mengine mtazidishiwa.
VIFUNGO VYA TABIA
Na Mch. Josephat Gwajima 04.03.2013
Utangulizi:
Shetani hajabadilika na silaha zake ni zilezile; na jambo kubwa linaloshangaza watu ni kwamba silaha za shetani ni zilezile lakini bado zinatenda kazi kwenye maisha ya watu. Moja ya kifungo kinachosumbua watu ni kifungo cha tabia.
Mara nyingi kupata urafiki au uhusiano ni rahisi lakini ili uweze kuendelea kuwa karibu na watu hao unatakiwa uwe na tabia nzuri. Hivyo shetani anaweza kukuacha usonge mbele na kazi ya Mungu lakini akakuzuia kupitia vifungo vya tabia. Kwasababu hii Roho Mtakatifu ametaka leo tujifunze kuhusu vifungo vya tabia:
KIPAWA NA TABIA YA MTU:
Kuna vitu kadhaa vya kuangalia kama mtu wa Mungu unayehitaji kufanikiwa, cha kwanza ni kipawa na pili ni tabia ya mtu.
Mithali 18:16 “zawadi ya mtu humpatia nafasi, humleta mbele ya watu wakuu; ” hili neno zawadi kwenye Biblia ya kingereza linaitwa “GIFT” au kwa Kiswahili kipawa. Sasa basi kipawa cha mtu chaweza kumfikisha mbele za watu wakubwa na kujulikana. Mfano mtu anaweza kuwa na kipawa cha uwimbaji lakini anakaa kijijini na umaskini, ila kile kipawa chake kikionekana kinaweza kumleta mtu huyo mjini hii ndio maana ya sehemu ya kwanza ya andiko hilo. Kwasababu hiyo kila mtu aliyepo duniani amepewa kipawa na Mungu ambacho kwa hicho anaweza kufika kwenye hatua ya juu zaidi.
Sasa basi kipawa cha mtu humleta mtu kwenye mafanikio yake, tatizo linakuja pale mtu anapokuwa na kipawa lakini tabia yake si nzuri. Hivyo tabia ndio ambayo inakubakiza katika sehemu uliyopo. Mtu anaweza kuwa na macho ya rohoni au upako lakini kama tabia yake ni mbaya hakuna mtu atakayetamani kuwa karibu naye. Ili Mungu akutumie kwa kiwango cha juu ni muhimu kuanza kwa kubadili tabia yako.
TABIA ZA KIMUNGU NA TABIA ZA ASILI:
Biblia imeainisha tabia za aina mbili, yaani tabia ya Kimungu na tabia ya kiasili au ya mwilini. Katika 1Wakoritho 2:14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” 1Wakorintho 3:1 kuna tabia za rohoni na tabia za mwilini. Hivyo anachosema Mtume Paulo ni kwamba unapoongea na watu inabidi ujue ama mtu huyo ana tabia za rohoni au za mwilini. Mfano mtu anaweza kuwa mwimbaji mzuri lakini ana tabia ya uongo; Mtu mwingine anaweza kuwa na kipawa kitakachomfanya apate mchumba; lakini kama tabia yake ni mbaya ama uongo, au umbeya au uzinzi inaweza kumfanya kuachwa na mchumba wake sio kwasababu hapendwi bali kwasababu ya tabia. Tabia ya Kimungu ni tabia njema na nzuri lakini tabia ya kibinadamu ni tabia mbaya aliyonayo mtu.
Shetani akitaka kuharibu kipawa cha mtu anaanzia kwenye tabia yake; kwa maana hiyo tabia ya kibanadamu au ya mwilini ndio hiyohiyo Biblia inaiita tabia ya kishetani. Ukisoma katika Yakobo 3:15 “Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani.” Unaona kumbe tabia mbaya ya kinadamu ndio hiyo inaitwa tabia ya kishetani. Mhubiri 10:1 “Mainzi mafu huvundisha marhamu ya mwuza marashi; Kadhalika upumbavu haba ni mzito kuliko hekima na heshima.” Hili ni neno la hekima la Mfalme Suleimani kusema mainzi wanaweza kuharibu marhamu nzuri; ikimaanisha unaweza kupata mpenyo katika maisha lakini tabia mbaya inaweza kukupeleka mbali kabisa na upenyo wako.
Ndio maana waweza kumkuta mtu ni mwombaji au anatenda miujiza lakini tabia yake ikawa mbaya kwasababu ya asili. Jambo hili ndlo linalosabisha watu wengine kusema “kama ulokole ndio huu sitaki kuokoka” kumbe mtu huyo aliwahi kumuona mtu ambaye ameokoka na ananena au anaombea watu lakini ni mwongo au mzinzi. Katika Biblia, Samson alikuwa mnadhiri wa Mungu na alikuwa amepakwa mafuta tangu tumboni mwa mamaye. Japokuwa alikuwa mpakwa mafuta lakini alikuwa na tabia mbaya ya kutaka wasichana wa kifilisti ambao Mungu alikataza tangu mwanzo. Hii ni sawa na mtu kung’ang’ania kufungwa nira na mtu asiyeamini. Kwa njia hii Samson akakutana na Delila ambaye lengo lake halikuwa upendo bali ni kumharibia kipawa chake kwa kuijua siri yake. Vivyohivyo shetani amewaangamiza watu wa Mungu wengi kwa kuwafanya waoe au kuolewa na watu wasiomjua Kristo na matokeo yake kile kipawa cha Kimungu kilichokuwa ndani yao kinashindwa kuonekana tena.
KUBADILI TABIA:
Tabia mbaya ya mtu huondoka kwa kuamua mwenyewe, hata kama mchungaji akuombee mara zote kama tabia yako ni mbaya kwa asili inakulazimu kuamua kuibadili mwenyewe. Ni kweli tabia yako inaweza kuwa imeshakupotezea kibali kwa watu au imeshakupotezea upenyo katika maisha lakini ukiamua kuanza upya na BWANA na kuacha zile tabia mbaya Mungu wetu ni wa nafasi ya pili. Mungu wetu anatoa nafasi ya pili biblia inasema, “usifarahi ee adui yangu niangukapo mimi nitasimama tena”
Leo naongea na watu ambao walikuwa waombaji leo hawaombi tena, walimuhofu Mungu lakini leo hawana hofu, walikuwa watakatifu lakini leo ni waovu wakubwa Mungu anayo nafasi ya pili kwaajili yako. Amua kutubu na kuacha dhambi na tabia hiyo mbaya; Mungu atakuwezesha tena kama alivyomwezesha Samson kuwaangamiza wafilisti wote. Hivyo uamuzi wa kwanza ni kuamua mwenyewe kuacha tabia hiyo
VIFUNGO VYA MWILINI
Na Mch. Josephat Gwajima 03rd March, 2013
Utangulizi:
Mungu anawapenda sana wanadamu na Biblia inasema wazi kuhusu hili katika kitabu cha Maombolezo 3:31; Ni raha yake kuona hatuna matatizo na tunaishi kwa amani. Mungu hakumuumba mwanadamu ateseke bali alimuumba afanikiwe akiwa duniani na kuishi kwa furaha.
Wakati huohuo, shetani kwa asili hapendi mtu aliyeumbwa na Mungu afanikiwe na ndio maana katika Luka 3:16 inasema, “…ambaye shetani amemfunga miaka kumi na minane…” (Matendo 10:38; 2Wathesalonike 2:18-19) kwa maandiko hayo tunaweza kujua kuwa shetani anaweza kufunga, kuzuia, kupinga na kushindana na mtu. Kwa asili shetani ni mshindani na furaha yake ni kuwatesa wanadamu ambao wanapendwa na Mungu. Yeye hufanya hivi ili kuumiza moyo wa Mungu kupitia wanadamu walioumbwa na Mungu.
SHETANI ANAWEZA KUMFUNGA MTU:
Kama tulivyoona kuwa shetani anapenda kuwatesa wanadamu na ili kutimiza lengo lake njia mojawapo anayotumia ni kuwafunga watu. Na tunapotaja vifungo, tunakuwa tunazungumzia vifungo vya aina kuu tatu, yaani, Vifungo vya mwilini, Vifungo vya rohoni na vifungo vya nafsini kwasababu mtu ni roho inayokaa ndani ya nyumba iitwayo mwili. Katika hatua hii ya kwanza tunaanza kuangalia kwa undani kuhusu vifungo vya mwilini:-
Mwili ni nini?
Hatuwezi kujua namna mwili unavyoweza kufungwa bila kujua asili ya mwili wa binadamu. Tuanze kwa kuangalia andiko hili Mwanzo 2:7 “BWANA Mungu akamfanya mtu kutoka katika mavumbi ya ardhi…” kumbe asili ya mwili wa mwanadamu ni mavumbi au udongo. Na ndio maana katika Isaya 64:8 Biblia inasema, “… sisi tu udongo nawe ni mfinyanzi wetu...” nabii Isaya ambaye aliwahi kumuona Mungu lakini alijua ukweli huu kuwa mwili ni mavumbi (Ayubu 7:21, 34:15). Kumbe pamoja na kuwa umevaa vizuri au umeupamba mwili vizuri lakini asili yake ni udongo na katika ulimwengu wa roho huonekana kuwa ni udongo kabisa. Kwa ufupi mwili wa mwanadamu ni udongo na mtu anapokufa mwili huirudia nchi (Mhubiri 12:7) yaani mavumbi.
Ndio maana hata watu wanapooana ni miili ndio ambayo inakuwa imeoana na si roho kwasababu mbinguni hakuna kuoa wala kuoana kule ni katika roho. Kwa kujua kuwa mwili ni udongo basi namna ambayo unaweza kuutendea udongo wa kawaida ndivyo vilevile waweza kuutendea mwili wa binadamu. Udongo wa ardhini waweza kuoteshwa mimea na kuchimbwa, vilevile na mwili wa binadamu waweza kufanyiwa hivyo.
TOFAUTI KATI YA MWILI NA UDONGO WA KAWAIDA:
Kuna mambo mawili makuu yanayosababisha mwili wa binadamu uwe tofauti na udongo wa kawaida.
1. Mwili uliwahi kushikwa na mikono ya Mungu maana hakuna kitu kilichowahi kushikwa na Mungu na kikabaki kama kilivyo.
2. Ndani ya mwili wa mwanadamu kuna roho ambayo huuisha mwili na kuupa uhai. Kwasababu hizo mwili wa mwanadamu hutofautina na udongo wa kawaida.
MWILI WA MWANADAMU UNAWEZA KUPANDIWA VITU:
Biblia iko wazi kuwa Mungu wa mbinguni anaweza kupanda, (Mwanzo 2:8); kumbe Mungu ambaye ni roho (Yohana 4:24) anaweza kupanda katika ardhi kabisa vivyo hivyo shetani naye ni roho naye ana uwezo wa kupanda katika mwili ambao kwa asili ni udongo. Hapa ndipo lile andiko la “KILA PANDO AMBALO BABA WA MBINGUNI HAKULIPANDA LITANG’OLEWA” linapoleta maana; Mapando ambayo hayajapandwa na Baba wa mbinguni ni lazima yatakuwa yamepandwa na shetani. Ndio maana ya mfano wa Yesu katika Mathayo 13:25 “lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.” Huyo ambaye Yesu anamwita adui ni shetani mwenyewe. Kumbe unapolala au kujisahau shetani huja na kupanda magugu, hili jambo linatendeka katika ulimwengu wa roho. Ni muhimu kujua siri hii kwamba kama vile udongo unavyopandwa vivyohivyo shetani naye anao uwezo wa kupanda juu ya mwili wa mwanadamu.
Unaweza kumsikia mtu analalamika kuwa mwili unachoma lakini kumbe katika ulimwengu wa roho mtu huyo amechomwa mkuki au kisu. Kufikia hapa sasa twaweza kujua kwanini Mungu alikataza kupanda mbegu mbili za tofauti katika shamba moja (Mambo ya Walawi 19:19). Mungu alisema hivi akitufundisha kuwa mahali ambapo Mungu amepanda shetani hatakiwi kupanda mahali pale. Mtu anaweza kuhisi vitu vinatembea mwilini kumbe amepandiwa wanyama wanaotembea katika mwili wake.
PEPO ANAWEZA KUJIGEUZA NA KUWA CHOCHOTE:
Tulijifunza kuhusu sheria mbili za rohoni, hapo tuliona uwezo wa pepo wachafu kujigeuza na kuwa kitu kingine yaani kuvaa sura mbali mbali ili kutimiza kazi zao. Jambo hili twaweza kuliona katika (1Wafalme 22:19-23) huyu pepo kwa asili hakuwa wa uongo lakini aliweza akaenda na akawa pepo wa uongo. Yule pepo akaingia katika vinywa vya manabii wa Mfalme Ahabu na kuwafanya wamtabirie uongo. Kwa maana hiyo tunaona uwezekano wa pepo mchafu kujigeuza na kuwa kitu chochote ili kutimiza lengo alilokusudia.
Sasa twaweza jua kuwa mapando tuliyokuwa tunayazungumzia ni pepo wachafu ambao hujigeuza na kuwa kile kitu na hivi ndivyo vinavyoitwa “Vifungo vya mwilini”. Wakati mwingine pepo anaweza kujigeuza na kuwa kinywa cha mtu, kama pepo wa katika (1wafalme 22:19-23) alivyofanya. Hivyo; unaweza kumuona mtu anatukana matusi ya ajabu bila hata aibu, kumbe pepo kajigeuza na kuwa kinywa chake. Pepo anaweza kuwa uso wa simba, unamkuta baba mwenye nyumba mkali kwa watoto na mkewe kumbe ni uso wa simba. Kwahiyo; pepo wanaweza kujigeuza maumbo mbalimbali kama nyani, simba, paka hata bundi ili mradi kuharibu hatma ya mtu. Mnamkuta dada aolewi kumbe uso wake umefunikwa kwa sura ya simba, kila mwanaume anayetaka kumchumbia haoni sura nzuri bali anaona simba. Na ndio maana kuna baadhi ya wadada watumia muda mwingi kujipodoa lakini bado hawapendezi kwa kuwa uso sio wa kwake.
KUNG’OA KILA KILICHOPANDWA KATIKA MWILI WAKO:
Imeandikwa kila pando asilolipanda Baba wa mbinguni litang’olewa, hivyo Mungu ametupa mamlaka ya kung’oa kila pando la kishetani yaliyopandwa katika mwili. Miili yetu ni Hekalu la Roho Mtakatifu hivyo shetani hatakiwi kugusa sehemu yoyote ya mwili wako.
Tumia mamlaka yako kung’oa kila pando ambalo shetani amepanda katika maisha yako mapando ya magonjwa, homa zisizoisha, ukimwi, mwasho wa mwili na matatizo mbalimbali. Jina la Yesu lina mamlaka yote dhidi ya kazi zote za shetani katika maisha yako.
Subscribe to:
Posts (Atom)